Tuesday, October 9, 2012

WATAKAO WATAJA WACHOMA NGURUWE KUPEWA KIFUTA JASHO

JESHI la Polisi Tanzania limetangaza zawadi ya Shilingi 150,000/= hadi 200,000/= kwa mtu au kikundi cha watu kitakacho toa taarifa na kufanikisha kupatikana kwa watu wanochoma mabanda ya Nguruwe Mjini Tunduru.

Zawadi hiyo imetangazwa na Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Ruvuma Bw. Deusdedit Nsemeki wakati akiongea katika kikao cha Viongozi wa madhahebu ya Dini, Wazee maarufu kilichofanyika katika Ukumbi wa Klasta Mjini hapa.

Akifafanua taarifa hiyo Kamanda Nsimeki alisema kuwa mtu au kikundi kitakacho zawadiwa kitita hicho ni kile kitakacho toa taarifa zitakazo fanikisha bila kuleta mashaka juu ya uhusika wa mlengwa katika matukio hayo ya kuharibu mali za wakristo yaliyojitokeza hivi karibuni Mjini humo.

Awali akiongea katika Mkutano huo kamishna kutoka Makao Makuu ya jeshi la Polisi Tanzania ACP.Rashid Seyf alisema kuwa nia ya kamati hiyo kuwaita makundi hayo ni kutafuta njia ya kuwapata wahalifu waliotekeleza matukio hayo huku akiwaasa kutumia lugha ya kuneneza ili kuondoa makwazo kwa kuwakumbusha machungu walioathiriwa na matukio hayo. 

Akitoa tamko kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Tunduru kaimu afisa Tawala wa Wilaya hiyo Bw. Manfed Hyera alisema kuwa pamoja na kupiga marufuku uuzaji na uoneshaji wa picha kutoka katika Cd,dvd ,hvc ,Flash na Memori Card zote zinazo kashifu dini nyingine pia Kamati ya Ulinzi na Usalama imeridhia kudhibitiwa muda wa ufungaji wa Vilabu vya pombe, waendesha Piki piki na taxi kumaliza shughuli zao saa 5 kwa siku za kawaida na saa 6 siku za mwisho wa wiki na sikukuu.

Alisema pamoja na maelekezo hayo pia uongozi wa wilaya hiyo umetoa maelekezo yatayotakiwa kufuatwa na wahubiri wa mihadhara ya kidini pamoja na  kuhakikisha kuwa kila muhubiri atafanya mahubiri yake chini ya ulinzi wa Polisi na kwamba kutakuwa na timu itakayo jihusisha na upigaji wa picha pamoja na kurekodi neno kwa neno kama ushahidi endapo muhusika atakiuka maelekezo hayo.

Bw. Hyera aliendelea kueleza kuwa pia Wilaya hiyo imehimiza kuanzisha ulinzi Shirikishi wa kutumia Sungungu huku wahudumu wa nyumba za kulala wageni wakihimizwa kuandikisha kwa ufasaha majina na anuani za wageni wote ikiwezekana wajiridhishe kwa kuomba na kusoma Vitambulisho vya wahusika zikiwa ni juhudi za Serikali kudhibiti matukio ya aina hiyo.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Bw. Chande Nalicho aliwataka wananchi kujenga tabia za kutoa taarifa za matukio mabaya ili kuisaidia serikali kuyadhibiti kabla hayajaleta madhala makubwa kwa jamii.

Wakichangia kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi walidai kuwa hali hiyo imetokana na ulegevu wa serikali kwa kushindwa kusimamia miongozo ya utengaji wa maeneo ya kuishi na kufugia hali ambayo ilitoa uhuru kwa Wananchi kuweka Mifugo yao katikati Mji na makazi ya watu huku vitendo vya uuzaji na uwekaji holela wa CD zinazo kashfu Dini nyingine kuwa ni miongoni mwa vichochea vya matukio ya uchomaji wa Nguruwe, Mazizi, Nyumba, Magari pamoja na uharibifu wa mali za watu.
.
 Wakielezea masuala ya uendeshaji wa dini kwa niaba ya waumini wa madhehebu ya kiislam Shehe Mkuu wa Wilaya hiyo Alhaji Waziri Chilakwechi na Askofu Mkuu wa Jimbo la TUNDURU- MASASI pamoja na mambo mengine waliunga mkono maamuzi ya kuzuiliwa kwa mikanda hiyo huku wakidai kuwa vitendo hivyo vinavyofanywa na kikundi hicho kwa mwavuli wa dini mbali na kutia aibu jina la Wilaya yao pia kinachafua haiba na uisilam na ukristo.

Bw. Rajab Rashid Mkwawa, Bw. Rashid Mkanyasine, Bi. Janneth Amani wakamweleza Mkuu huyo wa Wilaya kuwa kitendo cha Serikali kushindwa kuwakamata wahalifu hao kunatokana na suala hilo kuhusishwa na UDINI hali ambayo kila mtu anaogopa kulisemea.

Bw. Abdalah Kawanga, Ado Makanya pamoja na kuunyooshea vidole udhaifu wa vyombo vya Usalama hususani jeshi la Polisi ambalo hivi sasa limepoteza maadili kutokana na watendaji wake kuanza kutoa siri na kuwataja kwa wahalifu wanaotoa taarifa hizo za siri pia waliwatuhumu wazazi kwa kufumbia macho Lugha ambazo zimekuwa zikitumika na vijana wao kuwa endapo zitadhibitiwa ni rahisi kuwatambua wahusika.

Kufuatia hali hiyo wananchi hao wakaitaka Serikali kupitia Mkuu huyo wa Wilaya hiyo kutumia mamlaka waliyopewa kwa kuanza kuwachukulia hatua watendaji wote wanaoshimdwa kuwajibika ili kujenga nidhamu ya utendaji kazi na kurejesha imani ya upatikanaji wa huduma bora kwa jamii.

No comments:

Post a Comment