Wednesday, March 6, 2013

MKUU WA MKOA WA RUKWA AKAGUA MIRADI YA USIMAMIZI WA ZIWA TANGANYIKA (PRODAP) KATIKA HALMASHAURI YA WILAYA YA SUMBAWANGA


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya akiwa na msafara wake wakikagua ujenzi unaoendelea wa daharia (bweni) katika shule ya sekondari Kasanga. Mradi huo ni sehemu ya miradi inayofadhiliwa na mradi wa usimazi wa ziwa Tanganyika uliopo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira pamoja na miradi mingine ya ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika shule ya msingi Muzi na ujenzi wa wadi ya kujifungulia kinamama kijiji cha Samazi. Miradi yote hiyo itawanufaisha wakazi wa mwambao wa ziwa Tanganyika na inagharimu zaidi ya shilingi milioni 150.
 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Samazi mwambao na ziwa Tanganika alipofika kukagua ujenzi wa wadi ya kujifungulia kinamama katika kijiji hicho. Mkuu huyo wa Mkoa alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kuwafuatilia kwa karibu wahandisi wanaojenga miradi hiyo iweze kukamilika kwa wakati. Aliwaasa pia wananchi kuzingatia uzazi wa mpango katika kuboresha maisha yao pamoja na kuwaendelezea watoto wao kielimu tofauti na hali ilivyo hivi sasa ambapo muamko wa elimu Mkoani Rukwa upo chini. Aliwataka pia kuboresha hali ya ulinzi katika maeneo yao ya mipakani kwa kutokuwakaribisha wageni bila kuwa na taarifa zao za kutosha.
 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na msafara wake wakikagua ujenzi wa madarasa matatu katika shule ya Msingi Muzi yaliyowekwa jiwe la msingi na Naibu Waziri wa TAMISEMI Aggrey Mwanri ambayo mpaka kukamilika kwake yatagharimu zaidi ya shilingi Milioni 50. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya akizungumza na wanafunzi wa shule ya msingi Muzi iliyopo pembezoni mwa Ziwa Tanganyika Mkoani Rukwa baada ya kukagua ujenzi unaoendelea wa madara yanayofadhiliwa na mradi wa usimamizi wa ziwa Tanganyika mradi ambao upo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira. Aliwaasa wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kuwaahidi kuwapa ushirikiano wale watakaofaulu vizuri na kukosa uwezo wa kujiendeleza.
 
Sehemu ya fukwe ya Ziwa Tanganyika katika kijiji cha Samazi Mkoani Rukwa ambapo mradi wa usimamizi wa ziwa Tanganyika unatekeleza mradi wa ujenzi wa wadi ya kinamama kwa ajili ya kujifungulia katika Zahanati ya kijiji hicho.

No comments:

Post a Comment